Quantcast
Channel: TZhiphop » Swahili
Viewing all 10 articles
Browse latest View live

JCB ndani ya FidStyle Friday

$
0
0

Baada ya Cliff Mitindo kuwakilisha Migo Migo, wiki iliyofuata ilikuwa ni ya mkongwe JCB. Wanaomfahamu vizuri JCB nadhani watashauri ujiandae kupokea hadithi za kitaa kama zilivyo. Kama Mejah wa Wachata Crew anavyosema, JCB amekuwa akilinda ngome ya Kijenge Juu toka mwaka 1996, akihakikisha familia ya Watengwa inaendelea kufanya kile kinachotakikana — kuwakilisha mitaa, hasa Kijenge Juu.

Akionesha uzoefu wa hali ya juu mbele ya kipaza, anahakikisha kila mtu anajua kuwa yeye ndio yupo ndani ya nyumba! Lakini wakati huo huo anaambatana na taswira za kitaa, maneno yake yakiwa lenzi inayokuonesha kila kitu kinachoendelea Kijenge Juu (Donnie, familia ya Watengwa na Hip Hop Tanzania wanakusubiri).

Pia, JCB anatumia fursa hii kujadili mikakati yake na mipango ya Watengwa — “Ni Full Ile Laana Vol 2″ inakaribia kuingia kitaani — bila kusahau S.U.A. Kikosi cha CheusiDawaTV kitawatembelea Watengwa na kumhoji Daz Naledge ili kutupa undani na maendeleo ya mradi mzima.

Hadithi za kitaa…

Makala nyingine kuhusu JCB na Watengwa:


S.U.A. kuandaa Tamasha la Hip Hop

$
0
0

Juhudi na harakati za mradi wa S.U.A. (Saving Underground Artists) unaoendelea Kijenge Juu Arusha zimeanza kuzaa matunda, hasa katika upande wa kuwafikia vijana wengi zaidi kulinganisha na hapo awali.

S.U.A. wakishirikiana na Jambo Festival wanakuletea mashindano ya “freestyling” na “deejaying” yatakayokuwa yakifanyika kwenye uwanja wa wazi AICC club, Arusha. Tukio hili la siku tano litaanza tarehe 22 Oktoba na kumalizika tarehe 28 Oktoba, 2012. Kiingilio ni bure kama ilivyo desturi ya S.U.A.

Kutoka kushoto; Daz kutoka SUA, A. Kastrow (wa IDEA AFRICA) na G. Kway (wa K-Vant Gin).

Kwa taarifa zaidi, tembelea ukurasa wa S.U.A.

Exclusives Mix 10

$
0
0

Hii ni mix ya aina yake. Nakuonjesha mawe yaliyomo kwenye kazi za wasanii zilizoingia sokoni hivi karibuni. Kama ulikuwa bado hujazipata, basi bila shaka utajitahidi kuzitafuta baada ya kusikia sauti zinazobeba mistari hii…

Hatuna budi kutoa pongezi kwa kikosi kizima cha TamaduniMuzik, na tujitahidi kuwapa moyo kwa kununua nakala halisi za kazi zao!

Kurasa nyingine:

Kalapina ndani ya FidStyle Friday

$
0
0

Kikosi cha Mizinga ni mojawapo ya makundi muhimu mno ambayo yamekuwa yakiendelea kuwa na sauti muhimu kwenye medani ya Hip Hop Tanzania, huku wakiwa wameegemea zaidi kwenye kuwasilisha vilio vya watu wa tabaka la chini dhidi ya “wanyonyaji”.  Kikiongozwa na Kalapina, Kikosi  kimeendelea kujikusanyia wafuasi — tofauti na mashabiki — nchini na nchi za jirani, wakirusha mawimbi kutoka Block 41, Kinondoni, Dar es Salaam.

Katika kipindi cha FidStyle Friday cha wiki hii, tunapata fursa ya kusikia kutoka kwa Kalapina tena, akirusha mabomu kuelekea kwenye mifumo ya siasa. Pia, wasanii kama Zimwi, Aboo Gaidi na Onya Man, kutoka Kikosi Records, wanahakikisha ile sauti na nguvu inayohusishwa na Kikosi inasikika na kuonekana.  Fid Q na Kalapina wanajadili mambo kadhaa nyeti, kuanzia matatizo ya hati miliki hadi sanaa ya uandishi au ushairi — kuandika ambacho unahisi au kuandika unachofikiri?

Makala na kurasa zaidi kuhusu Kikosi:

Nikki Mbishi ndani ya FidStyle Friday

$
0
0

Hiki ni kipindi cha 30 tangu maneno “FidStyle Friday” yalipoanza kusambaa kwenye mtandao. Katika kusheherekea hatua hii muhimu, ni vyema kuangalia kilichokuwa kinajiri awali.

Nikki Mbishi alikuwa ni msanii wa kwanza kualikwa, na anaalikwa tena ili kutumia darubini yake kuangalia safari ilipoanzia. Kama kawaida, Nikki hajaharibu; anafungua kwa Sauti ya Jogoo kuamsha jamii nzima ya Tanzania, kuanzia tabaka la juu mpaka la chini kabisa na kukumbusha watu majukumu yao. Mfalme wa “underground mainstream” pia anaongelea jinsi uhalisia, na wasanii wanaoakisi uhalisia, unavyowapa taswira bora mbele ya hadhira na jamii kwa ujumla.

Ukiacha mjadala na Fid Q kuhusu Hip Hop na sanaa Tanzania, Nikki anaonesha kipaji alichonacho cha kutunga na kuwasilisha ushairi. Ingawa kuna wakati anaongelea mambo ambayo labda hayajadiliwi au hayaongelewi kwa “uwazi”, ni wazi kuwa Nikki anajua anachofanya. Msikilize kwa makini jinsi anavyocheza na maneno. Mfano mzuri ni mstari huu kutoka kwenye wimbo Kilinge: “Hata ukiwa na mvi Shirazi unahitaji Afro.” Au: “Nageuka Oliver, Mtukudzi namwimbia Tobi na Neria.” Unaweza ukadhani anasema, “Nageuka Oliver, mdokozi namwibia Tobi na Neria!”

Mistari kama hiyo ya kutega akili ipo mingi tu, kwa hiyo mtegeee sikio huyu Drosophila melanogaster kwa makini. Mtiririko wa maneno yafuatayo kwenye mojawapo ya beti anazowasilisha utakuacha unatingisha kichwa: “Nini Chanzo… Hili Game… Juma Nature.”

Taarifa na makala zaidi kuhusu Nikki Mbishi:

Kichupa cha ‘In The Congo’

$
0
0

Ndugu Zavara, mmoja wa waanzilishi wa Bongo Hip Hop na waasisi wa kundi la Kwanza Unit, anagusia vita ya Kongo katika ‘In The Congo‘ kwa mtindo wa kipekee kwenye kichupa hiki adhimu. Pamoja na wimbo huu kugusia vita mas-ala ya maafa ya vita Kongo, halkadhalika kuhomola (kwiba kwa “Kitemeke”) utajiri wa madini ya huko kwa ndugu yetu wa Msasani, bwana Josefu Kabila.

Zavara kwa umakini bila kupitiliza  amefanikiwa kuinakshi mandhari ya kichupa, kwa muundo tofauti kabisa na hivi vya siku zote hapa Bongo. Madini husika, yanayoendeleza ukatili angamizi wa Mfalme Leopold ni madini ya coltan, yanayotumika kutengezea vifaa vyetu vya elektroniki. Hata hivyo, vita ya Kongo inasababishwa na mwingiliano wa mambo mengi, kutokana na utajiri wake wa madini na historia ya nchi hiyo.

Nyimbo inashirikisha wasanii wa kike, kama mwanaharakati na mahiri sana wa mitindohuru toka jiji la Tofaa Bovu (New York), Toni Blackman (aliyepewa wadhifa wa balozi wa US Hip Hop), akishirikiana na kundi lake la Rhyme Like A Girl, pamoja na mwanadada mzaliwa wa jiji la Malkia Bi’ Khalifa (siku hizi Kalifonia) mwenye asili ya Kenya, Nasambu. Huu upangaji katika ushirikishwaji una umuhimu. Bado sijui kama Zavara alidhamiria kushirikisha wasanii wa kike tu, au ilitokea bila kukusudia. Hii ina umuhimu wake, hasa ukizingatia maafa ya Kongo pamoja na kuendelea kuuawa kwa halaiki ya watu, ubakaji uliokithiri umeacha wanawake wengi na makovu. Hivyo, kuona muungano wa sauti za akina dada katika ‘In The Congo’ inatia imani na faraja kuwa kuna wanaojali.

Mpangilio wa washirikishwaji katika ‘In The Congo’ unaweza kutazamwa kama kichaka cha saruji (New York) ukutanapo na misitu ya Kongo, wanapopigana wanajeshi na waasi. Vita hii inaendeshwa na ulevi wetu wa vifaa vipya vya elektroniki, kama simu za mikononi, kompyuta za kupakata na kadhalika, huku Wakongo wakijikuta wamebanwa katikati ya risasi za wanajeshi na waasi wanao faidika na mauzo ya madini hayo ya coltan. Wakongo wengi wanaweza kutojua madini hayo yanatumiwa kwenye nini hasa, lakini wanajua fika jinsi gani vita hii inayosukumwa na mauzo ya madini hayo inavyoendelea kuathiri maisha yao.

Mimi kama Mtanzania, na mpenzi wa muziki wa Hip Hop, nafurahi kuona Waafrika wengine wakijiunga katika kutuhabarisha juu ya vita hii, kwa kupitia nguvu ya kinasa na mashairi ya Hip Hop. Ujumbe ni rahisi, hauchochei watu kugoma kutumia vifaa hivi vya elektroniki, lakini kuwa makini, kwa kununua vile ambavyo havichochei maafa zaidi na ambavyo vinakuza haki katika biashara. Hii itasaidia kuokoa maisha ya Wakongo wengi. Ni matarajio kuwa ujumbe umefika, na hivyo kutusukuma mimi na wewe kuchukua hatua. Hii ni muhimu, hasa tukizingatia Afrika ndio soko linalokuwa kwa kasi ya vifaa kama simu za mikononi, ambazo ndio zinatengenezwa na madini hayo ya coltan kutoka Kongo.

Bofya hapa kujipatika nakala ya wimbo ‘In The Congo’.

Watengwa 2 France, Musical Safari

$
0
0

Watengwa‘s highly anticipated album, Ni Full Ile Laana Vol. 2, is about to hit the stores (be on the look out for the exact date). The album was recorded, mixed and mastered in Paris, France, during the East Africa Rise Up tour last year. While they were at it, Watengwa prepared a documentary showcasing how the tour went, the recording sessions, etc.

… Here is the first part of the documentary, aka Watengwa 2 France, A Musical Safari Part 1 (Subsequent parts will be posted here; one every week):

Watengwa 2 France, A Musical Safari Part 2:

Related posts and pages:

Uchambuzi: Fid Q – Siri Ya Mchezo [I]

$
0
0

Uhakiki na Jicho La Ra

Siri ya Mchezo ni wimbo mwingine kutoka kwenye santuri mpya ya Fid Q inayoitwa Kitaalojia. Ukisikiliza vizuri, utunzi wa wimbo huu ni kama unataka kushabihiana na ule wa “Propaganda”. Maudhui ya Siri Ya Mchezo yanagusa sehemu kuu mbili. Moja ni tasnia ya muziki, hasa huu wa kizazi kipya na pili ni ulingo wa siasa. Tasnia ya muziki inamgusa Fid Q mwenyewe moja kwa moja, ingawa si hivyo na siasa kwani yeye sio mwanasiasa. Mashairi yake lakini ni mashairi yenye uanaharakati, yaani “political consciousness”.

siri ya mchezo

Mdundo wa Siri ya Mchezo ni wa kawaida, labda kwa sababu Fid alitaka tusikilize mashairi zaidi kuliko mdundo. Kiitikio cha Juma Nature kwa mtazamo wangu kingependeza zaidi kama kingepambwa na sauti ileeeee kama ya kwenye Sonia, iliyokuwa na mahadhi kama ya kaswida kaswida hivi.

Denzel Washington wa Cry Freedom, ndiyo yule Steve Biko wa Afrika Kusini?

Kitu kinachovuta hisia zangu kwa karibu zaidi katika mstari wa kwanza ni jina la Biko. Marehemu Steve Biko alikuwa mwanaharakati wa haki za watu weusi wa Afrika ya Kusini dhidi ya utawala wa makaburu. Biko alihamasisha watu weusi kujipenda wenyewe, “black is beautiful”. Fid anaghani, “stimu zikanipa elimu ya Biko”. Elimu ambayo Fid anazungumzia ni hii ya uanaharakati, kwani Biko kitaaluma alisomea udaktari. Mashairi ya Fid nayo yanatetea haki za wanyonge dhidi ya tabaka la wanyonyaji, mfano viongozi wala rushwa na mafedhuli, au kwa jina jingine, wafadhili — wafadhili wa “ukoloni mambo leo”.

Fid haoni aibu kuweka bayana uwerevu wake wa mambo “wanapagawa na baadhi ya mambo nayoyajua”. Kwa mfano, wangapi tulimfahamu Biko kabla ya Fid kumtaja? Fid anaposema “elimu ya Biko”, mimi inanipa maana mbili tofauti. Maana ya kwanza ni mbinu alizotumia Biko kufanya uanaharakati wake. Ukifanya utafiti utagundua Biko hakufundishia darasani, bali alifanya uanaharakati kwa njia ya mihadhara tena kwa kujificha.

steve bikoSasa swali ni, je, Fid na yeye anatuelimisha na uanaharakati wake kwa njia ya nyimbo zake kama Biko alivyofanya na mihadhara yake? Elimu hiyo ya Biko ndio iliyohamasisha Kitaalojia? Inawezekana nyimbo za Fid ni zaidi ya burudani, bali ni mihadhara pia, au elimu isiyo rasmi (informal education). Falsafa ya Biko ilikinzana na elimu ya makaburu ambayo ilichochea ukandamizaji. Je, elimu yetu mashuleni inafanana na hiyo ya makaburu kwa kudumaza uwezo wa kuchanganua mambo na kufikiri, ukilinganisha na elimu iliyomo ndani ya mashairi ya Fid Q ambayo yanathubutu kutulazimisha kufikiri?

Maana ya pili ya “elimu ya Biko” kama nilivyoelewa, utagundua, pamoja Biko alisomea udaktari, lakini uanaharakati wake ulimpeleka kwenye siasa pia; “black consciousness”. Biko alikuwa mwerevu wa sheria pia, pamoja haikuwa taaluma yale, lakini alijisomea mwenyewe mpaka akawa gwiji. Hapo unaweza kuona jinsi Fid Q alivyofuata nyayo za Biko. Pamoja Fid ni msanii, lakini anajua mambo mengi kama sosholojia, siasa na mambo mengineyo kwa kujisomea tu mwenyewe.

Lakini Biko ameathiri kwa kiasi gani maisha ya Fid Q? Biko amemsukuma Fid afanye nini zaidi ya kuandika mashairi ya uanaharakati? Kwani, pamoja ya kwamba Biko aliandika hotuba kali, kama Fid na mashairi yake, Biko alikuwa mstari wa mbele kupigania haki kwa vitendo, na ndio huo ujasiri uliopelekea kuuwawa kwake na utawala wa makaburu. Ni muhimu tuelewe kuwa, kujua (awareness) ni kitu kimoja, na kutenda (to act) ni kitu kingine.

Kwenye ubeti huo huo wa kwanza, Fid Q anaturudisha kwa mwanaharakati wa hapa nyumbani. Almasi ya Bandia na kitabu cha Makuwadi wa Soko Huria, ni vitabu vilivyoandikwa na Marehemu Professa Chachage. Hapa tena, Fid anazidi kuonyesha uwezo wake wa kujua mambo kupitia upenzi wake wa kujisomea vitabu. Elimu haipo tu darasani kama wengi tunavyofikiria. Kwa upeo aliokuwa nao Fid, lazima ujiulize ni mantiki gani ilitumika na viongozi katika hoja yao iliyodai kuwa, vitabu vingi (riwaya za kufundishia fasihi) mashuleni vinachanganya wanafunzi na sio kuwaongezea maarifa.

Kitabu cha Makuwadi wa Soko Huria kinachanganua utandawazi, au kama ujulikanavyo siku hizi, utandawizi. Mawazo na nasaha za Chachage kuhusu utandawazi ni kali, hivyo ni changamoto kwako msomaji kukitafuta hicho kitabu na kujisomea mwenyewe.

makuwadi1

Katika mstari wa “zawadi ya almasi ya bandia”, mimi nilijikuta nikikumbushwa ile hadithi aliyosimulia Mwalimu Nyerere kuhusu Zuzu. Zuzu alikuwa na almasi ya kweli, kwa bahati mbaya au nzuri, alitokewa na mtu aliyekuwa na kipande cha chupa. Yule mwenye kipande cha chupa alifanikiwa kumshawishi Zuzu, mpaka Zuzu aliamini kwamba almasi yake ilikuwa almasi ya bandia, na kipande cha chupa cha yule bwana ndio almasi halisi. Masikini Zuzu alikubali kubadilishana, akiondoka na furaha akifikiri amepata kumbe yeye ndiye aliyepatikana. Unadhani hadithi hii inaakisi ukweli baina yetu sisi na wawekezaji?

Mistari ya mwisho ya ubeti ya kwanza inaanza kukupa picha ni jinsi gani kitabu cha Chachage kimemgusa Fid Q. Anaghani kwa kusema, “taifa la kondoo huendeshwa na serikali ya dubu”. Hapo lazima ushikwe na hamu ya kutaka kujua dubu ni mnyama mwenye tabia za aina gani. Matumizi ya kondoo hapa yanaweza kukufanya ufikirie Biblia, Yesu na kondoo wake. Kondoo huchungwa, na leo hii wachungaji wenyewe ndio hawa viongozi ambao wamekosa uaminifu. Wakati Yesu alichunga kondoo zake, hawa miungu watu wanatutupa kwenye vinywa vya  “mabepari” ambao hawana tofauti na “mbwa mwitu”.

Mwisho wa ubeti Fid anarudi kwenye utetezi wa vijana. Huu ukoloni mambo leo “unafanya vijana wanaumia”, Fid anaghani. Hapa inaweza kuwa ni suala zima la vijana kuzidi kukosa nafasi, kwani madhara yake yanaweza kuwa makubwa. Imam Abbas kwenye Bila Sanaa anaghani kwa kusema, “vibaka wa leo ni majambazi wa kesho”. Rick Ross pia kuna wimbo anaghani kwa kusema, “if I’m low on funds, I’m a load up guns”. Haya si maneno mepesi, hasa tukizingatia tayari kumepatikana kambi za kufundisha vijana ugaidi hapa Tanzania.

Mstari wa mwisho kabisa, anasema vijana “tunaishia kufia mabatani kama nzi ndani ya chupa ya bia”. Fid anazungumzia watu wanaokufa kwenye starehe. Hii inaweza kutokana na ukweli kuwa kwenye starehe hakukosekani mambo au vitu vya anasa. Huu utamaduni wa kupenda starehe sisi vijana ndio tumeupa kipaumbele kuliko mambo ya msingi. Taswira ya nzi katika chupa ya bia inanikumbusha wimbo wa Kendrick Lamar “Swimming Pools”.

Lakini je, inawezekana vijana tunapenda kupombeka (ulevi) kutokana na kukosa imani na maisha yetu ya baadae, hivyo misongo ndio inayotupelekea tuwe walevi?

Mara ya kwanza niliposoma mstari wa “kufia mabatani”, nilidhani ni mabatini, hivyo tafsiri yangu ya haraka haraka, nilidhani Fid Q anazungumzia kituo cha polisi cha Mabatini, Sinza. Sasa tafakari, kama vijana wengi hawana ajira (sababu moja ya misongo ya vijana), na kuzurura ni kosa kisheria, basi ukweli ni kuwa wengi tutajikuta tumelundikwa polisi Mabatini.

Lakini kinachotisha zaidi ni utekelezaji wa sheria. Fid anaposema kufia, anaweza kuwa akimaanisha hivyo hivyo, kufia Mabatini. Kuna hadithi nyingi za vijana wanakamatwa kwa kosa la kuzurura, lakini wanaishia kubambikiziwa kesi kubwa kama za mauaji, na kujikuta wakisota jela kwa miaka mingi, wakitumikia vifungo vya watu wengine. Mfumo wa sheria umeathiriwa na rushwa. Hili suala la rushwa tutaendelea kulijadili kwenye sehemu ya pili, tuone ni vipi linaunganisha tasnia ya muziki na siasa — kwani hiyo ndio inaweza kuwa ni moja ya siri zilizojificha kwenye mchezo mzima.

 

Makala za Prof. Chachage:


One on One: WAKAZI

$
0
0

Kwa Wakazi, EP ya Abacus ni muendelezo wa safari ya kuelekea kwenye santuri yake. Wakazi ameshaonyesha uwezo wake kama msanii kupitia kanda zake tatu za mseto za MYU na Utatu Mtakatifu. Utatu Mtakatifu ndiyo kanda mseto bora kati ya zote tatu. Ndiyo kanda inayofunga mfululizo mzima wa kanda za mseto za MYU. Tofauti na zile za MYU, Utatu Mtakatifu ilisambazwa mtaani wakati za MYU zilisambwazwa mtandaoni peke yake.

EP ya Abacus ina nyimbo tisa ambazo ni ‘original’ kutoka kwa Wakazi mwenyewe. EP hii ni kiamsha hamu “teaser” ya santuri ya Wakazi inayotazamiwa kutoka hapo baadae. Wakati Abacus ikiwa imeshatoka, Wakazi anaendelea kutamba na nyimbo zake nyingine mpya kama “Sexy Lady”, “Touch” na “Sumu ya Panya” ambazo hazipo kwenye EP ya Abacus.

Mbali na Abacus, Wakazi anazungumzia pia mambo mbalimbali kuhusu hiphop hapa nyumbani, uandishi wa mashairi na mambo mengi mengineyo. Kwa msanii mchapa kazi “workethic” kama Wakazi, safari ndiyo kwanza imeanza.

Enjoy..

Kurasa nyingine muhimu:

Harakati

$
0
0

Sehemu ya makala hii imetafsiriwa kutoka kwenye gazeti la NYTimes moja na mbili

Rais wa Senegal Mh. Abdoulaye Wade aliwahi kutaka kubadilisha katiba ya nchi hiyo ili kufanikisha azma yake ya kugombea urais awamu ya tatu. Rais huyo ambaye alikuwa ameshajenga sanamu kubwa kwenye mji mkuu wa nchi hiyo lililogarimu milioni 27 za Kimarekani na kununua ndege mpya ya rais, uamuzi wake wa kutaka kubadilisha katiba ulizidi kuwakwaza wananchi wa Senegal.

Wakati wanasiasa wakisuasua kuikabili serikali ya Wade, wasanii wa hip hop Fou Malade (Malal Talla) na Thiat (Cheikh Oumar Cyrille Toure) walipanga na kuongoza maandamano ya vijana katika mitaa mbalimbali ya mji huo wa Dakar kupinga njama hizo za rais Wade.

Y’En A Marre

Wakati harakati zikiendelea mtaani, Thiat aliwekwa chini ya ulinzi na polisi kwa shutuma za kumkashifu rais wa nchi hiyo kwenye maandamano kwa kusema “mzee wa miaka 90, na aliye muongo, hana nafasi katika nchi hii”. Baada ya malalamiko kutoka kwa vyombo vya habari na waandamanaji, Thiat aliachiwa huru.

Mwamko wa wananchi, ulichangiwa sana na mashairi ya uwazi ya wasanii  hao bila ya kuficha ficha, tofauti na lugha ambayo hutumiwa na wanasiasa wengi. Uwezo wao wa kuzungumzia masuala nyeti bila kupindisha kauli au kutumia mafumbo, ndicho kitu ambacho kilivutia watu wengi hadi kuamua kuwaunga mkono. Hili la kutumia lugha ya uwazi – bila uwoga, bila uongo - ni moja ya sifa ya mashairi ya hip hop.

Harakati zao zilijulikana kama Y’En A Marre (Fed Up – Tumechoka). Wanaharakati hao walifanikiwa kuweza kumzuia rais Wade kugombea tena. Lakini ni vipi harakati zao ziliweza kufanikiwa?

Kundi la hip hop la Mr. Toure na harakati zake zilijikita kwa miezi kadhaa wakihamasisha watu kujiandikisha kupiga kura, ili kuwezesha hasira zao dhidi ya serikali ya Wade kusikika kwa kupitia kura zao. “Wewe sio raia kama hauna kadi ya kupigia kura” ilikuwa ni moja kati ya ujumbe waliotumia kuhamasisha wananchi.

Nyerere akisimama kwenye mstari kwenda kupia kura na Watanzania wenzake

Picha ya kulia: Mwl Nyerere akiwa amesimama kwenye mstari kwenda kupiga kura pamoja na Watanzania wenzake.

Pamoja kikundi hicho kilikuwa na makao makuu yake Dakar, ambapo vyama vya upinzani vinawafuasi wengi, harakati za wasanii hao zilibaki kuwa huru, bila ya kufungamana na chama chochote cha siasa. Harakati hizo ziliendelea kubaki mtaani, sehemu walipo walalahoi, sehemu ambapo ndipo harakati hizo zilipozaliwa.

Kilichotokea nchini Senegal ni mfano mzuri wa nguvu ya umma katika kuleta mabadiliko. Pia huu ni mfano mzuri wa jinsi hip hop ilivyo na uwezo mkubwa na muhimu katika kuchochea harakati. Hivi karibuni kumekuwa na mijadala mbalimbali kwenye mitandao ya kijamii kuhusu harakati na hip hop. Hii ni mijadala mizuri, inayodibi iyambatane na vitendo.

Wakati Tanzania tunajiandaa na uchaguzi mkuu mwakani (2015), ni muhimu tukijifunza kutoka kwa wengine, kama Senegal. Neno harakati sio lazima limaanishe fujo. Kitu cha kuzingatia kutoka kwenye harakati za Y’En A Marre ni kuwa hawakufungamana na chama chochote cha siasa, bali na wananchi.

Waandaaji na viongozi wa harakati za Y’En A Marre waligundua tangu mwanzo kabisa kuwa, serikali ina polisi na jeshi ambao wote hubeba silaha, lakini wao wanaungwa mkono na wananchi wenye kura, ambazo zina nguvu ya kutosha kuleta mabadiliko kwa kuchagua viongozi makini.

Matokeo ya uchaguzi mkuu wa rais:

Matokeo ya uchaguzi

Asilimia ya wapiga kura imeshuka kutoka 72.41% (2005) mpaka 42.84% (2010). Changamoto ndiyo hizi.                                                                                                                            Chanzo: idea.int

Wimbo huu wa “haki” una nafasi ya kuweza kuangazia mwanga sio tu haki za wasanii, bali haki za Watanzania wote, hasa masikini katika hii katiba mpya. Hivyo ikawa sio “haki” tu ya wasanii, bali “haki’ za Watanzania kwa ujumla, na hata kusaidia kuhamasisha vijana kuelewa mchakato mzima, na kuelewa haki zao na majukumu yao kama Watanzania kwa mujibu wa katiba.

Majukwaa yenye nguvu ya kuchochea harakati za upiganiaji haki na pia hata kusukuma wananchi kujielimisha kuhusu masuala ya nchi, kama katiba siyo mengi. Hapo zamani Chuo Kikuu cha Dar Es salaam (UDSM) kilikuwa ni sehemu moja wapo. UDSM ilikuwa ni sehemu ya mijadala mikali iliyoibua mitazamo tofauti kama ile iliyopatikana ndani ya jarida la cheche. Kilichofanywa na wanazuoni wa kipindi hicho, ni mfano mmoja wa kinachotegemewa kufanywa na kazi za fasihi. Kwa mtazamo wangu hip hop ina nafasi hiyo kama siyo jukumu hilo.

Emcee nina ubongo umbo la Nkrumah/ wenye vina vyenye cheche kama darasa la chuoni…

Nkrumah Hall, UDSM

Lakini labda ninategemea mengi sana kutoka kwa wasanii wa hip hop, wakati wengi wao wanakabiliana tayari na changamoto nyingi za maisha na sanaa zao. Kama siyo la umamluki wa media, basi hili la sheria kutolinda haki za kazi zao na mengi mengineyo. Ndio maana wimbo wa “haki” ni mwanzo mzuri wa safari ya kupigania haki kwa jamii nzima. Kama Senegal waliweza kwanini sisi tushindwe.

Lakini nina wasiwasi kidogo kutokana na utofauti wa jamii yetu na ile ya Senegal katika suala la mshikamano, hivyo kuweza hata kuhatarisha nguvu ya harakati za wana hip hop wa “haki”. Kwa mfano, wakati wananchi wa Mtwara walipoanzisha harakati zao dhidi ya serikali juu ya mabomba ya gesi, ni Watanzania wangapi waliwaunga mkono Watanzania wenzao? Au hata kuungana kupinga vitendo  vya uvunjwaji wa haki za binadamu vinavyosemekana kufanywa na vyombo vya dola dhidi yao. Ni tabia kama hii ya kupenda kuwa watazamaji badala ya washiriki, ndiyo ambayo inanipa wasiwasi.

Tuna uwezo wa kufanya mabadiliko au tunaweza kubaki tukihamaki na kuhemkia matokeo yasiyo na tija kwetu wala kwa nchi. Kwani bila kufanya mabadiliko, msuli utabaki kuwa tembo huku matokeo yakiendelea kuwa madogo kama sungura kama alivyosema Nikki Mbishi.

 Makala nyingine mhimu: 

Viewing all 10 articles
Browse latest View live